Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefiwa na dada yake, Monica Joseph Magufuli aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Monica amefariki leo August 19 ikiwa ni siku moja tangu Rais Magufuli amtembelee katika chumba cha uangalizi maalum hospitalini hapo.

Akitoa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kupitia akaunti zake za kijamii ameandika ujumbe ukiambatana na picha ya dada huyo wa Rais Magufuli akisema;

“Nasikitika kuwajulisha kuwa Dada wa Rais (John Magufuli), Monica Joseph Magufuli amefariki dunia leo Agosti 19, 2018 katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa akipatiwa matibabu,” amesema Msigwa.

“Natoa pole kwa Rais John Pombe Joseph Magufuli, familia ya Mzee Joseph Magufuli, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu,” ameongeza.

Msigwa amemaliza kuandika ujumbe wake akisema;

“Raha ya milele umpe e Bwana na mwanga wa milele umuangazie, marehemu Monica Jospeh Magufuli astarehe kwa amani, Amina.”

Dar24 Media tunatoa pole kwa Rais Magufuli pamoja na familia yote na Mungu awape faraja katika kipindi hiki. Amen

Lukuvi kumaliza matatizo yote ya ardhi Tabora
Video: Mitandao yamkamatisha Mmarekani aliyempiga vibao mhudumu