Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa kinapanga kufanya ziara visiwani Zanzibar kukagua ofisi za matawi yake ambazo imedai zimebadilishwa rangi kuwa za ACT- Wazalendo.

Akielezea mpango huo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana, Machi 21, Makamu Mwenyekiti wa CUF upande wa Zanzibar, Abbas Juma Mahunzi, amesema kuwa ziara hiyo itafanyika na kwamba watazirudisha ofisi za matawi yote ya chama hicho zilizofanyiwa kile alichokiita vurugu za kupakwa rangi.

Alieleza kuwa kupakwa rangi kuwa ACT-Wazalendo sio sababu ya matawi hayo kutokuwa ya CUF na kwamba muda ukifika watayachukua.

“Kitendo cha kuyapaka rangi kuwa ya ACT-Wazalendo haina maana kuwa sio ya kwetu, muda ukifika tutayatembelea na tutafanya hivyo [tutayachukua],” alisema Mahunzi.

“Tunafahamu watatutia hasara ya kuyabadili rangi matawi yetu, lakini haitajalisha kitu kwani tunajua wanachokifanya bado hawakielewi,” aliongeza.

Mabadiliko ya zilizokuwa ofisi za CUF kuwa za ACT-Wazalendo yalitokana na hatua ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na ACT-Wazalendo.

Akizungumzia hatua za kubadili rangi kwa ofisi hizo, Maalim alisema kuwa ofisi nyingi za CUF zilikuwa nyumba binafsi za watu ambazo walipewa kwa hisani hivyo ni hiari ya wenye nyumba hizo kufanya mabadiliko wayatakayo.

“Kama CUF wanataka kwenda kuzichukua, waende tu wakazichukue,” alisema Maalim Seif.

Marekani yashusha rungu jingine kwa Korea Kaskazini
Mama atembelea ndege ilipoanguka kila siku, sababu…

Comments

comments