Aliyekua nahodha wa kikosi cha Nigeria na kiungo wa zamani wa Chelsea John Mikel Obi, ameondoka kwenye klabu yake ya Trabzonspor, baada ya kupishana kauli na uongozi wa klabu hiyo, kufuatia janga la maambukizi ya virusi vya Corona.

Mikel amechukua maamuzi ya kuondoka klabuni hapo, kufuatia ombi lake la kutaka kusitishwa kwa muda ligi ya nchini Uturuki kupitia viongozi wake kudharauriwa, huku ligi mbalimbali duniani zikiwa zimesimamishwa kwa lengo la kuepuka maambuziki ya virusi vya Corona.

Ligi ya Uturuki bado inaendelea kwa sharti la michezo kuchezwa bila ya mashabiki, jambo ambalo linapingwa na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32.

Mikel, ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa, hakubaliani na utaratibu wa kuendelea kwa ligi, ili hali dunia nzima imeonyesha kuguswa na kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Jumamosi, Mikel aliandika kwenye ukurasa huo: “Kuna maisha zaidi ya soka” “Siwezi kuwa na amani wakati dunia nzima inapiga vita maambukizi ya virusi vya Corona.”

“Kila mmoja anapaswa kuwa nyumbani na familia yake. Msimu wa ligi unapaswa kusimamishwa ili kudhihirisha kwa vitendo, kuunga mkono harakati za kupiga vita janga hili.”

Kufuatia hali hiyo, uongozi wa klabu ya Trabzonspor leo jumanne umetoa taarifa za kusitisha mkataba wa kiungo huyo, na kumlipa marupurupu yake ili kumuwezesha kuwa mchezaji huru.

Mikel alijiunga na Trabzonspor mwaka 2019 kama mchezaji huru akitokea Middlesbrough  inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini England.

Alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu hiyo inayoongoza msimamo wa ligi ya Uturuki kwa sasa.

Video: Ni haramu mgonjwa wa Corona kuingia Msikitini - Mufti
Mgonjwa wa Corona aongea kwa mara ya kwanza "Naomba msamaha"

Comments

comments