Shirikisho la soka nchini TFF, limetangaza kusimamisha ligi zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa COVID 19 ambao umeingia nchini.

Taarifa ya TFF imeeleza kuwa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kilichoitishwa na Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia leo kitafanyika kama kawaida kesho Saa 3:00 asubuhi hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam, lakini kwa lengo la kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu.

Ligi Kuu inasimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 71, wakifuatiwa na Azam FC alama 54 baada ya wote kucheza michezo 28, wakati vigogo Young Africans ni wa tatu kwa alama zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za michezo 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC wenye alama 22 za michezo 28, Alliance FC alama 29, michezo 29, Mbeya City alama 30 michezo 29 na Ndanda FC alama 31 michezo 29.

Wakati huo huo TFF imethibitisha kuvunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilikuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon.

Breaking News: Wagonjwa wawili wa CORONA waongezeka Tanzania, vyuo vyote vyafungwa
CORONA: Serikali yasitisha michezo nchi nzima

Comments

comments