Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, amesema serikali imesitisha masuala yote yanayohusu mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima ikiwa ni kujikinga na ugonjwa wa Corona.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema hayo wakati akitoa msimamo wa Serikali kupitia vyombo vya habari kuhusiana ugonjwa huo.

Majaliwa amesema:-“Tumesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama vile Ligi Kuu ya Tanzania, Ligi Daraja la Pili, Ligi Daraja la Kwanza, lakini pia michezo ya shule za msingi (Umitashumta), michezo ya shule za Sekondari (Umiseta) pamoja na ile ya mashirika ya umma. Michezo yote hiyo imesitishwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo.

“Kwa hiyo Wizara ya Habari na Utamaduni na Michezo yenyewe itawaandikia mashirikisho yake yote ya michezo ili kuwaambia kwamba kwa kipindi cha mwezi mmoja hiki watatakiwa kusimamisha ratiba hizo katika michezo inayochezwa kipindi hiki.”

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema kuwa Serikali imeendelea kufuatilia abiria wanaoingia nchini kupitia maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani, kwa kuwapima abiria ili kubaini kama wanamaambukizi, sambamba na kuimarisha maabara ili iweze kupima na kutambua endapo kuna maambukizi.

“Tumetenga kambi maalum eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam, kituo cha afya cha Buswelo huko Mwanza, hospitali ya Mawenzi ya mkoani Kilimanjaro pamoja na hospitali za Mnazi mmoja, Zanzibar na Chakechake huko Pemba, ambazo zitatumika kuhudumia wagonjwa wa Corona” alisema Waziri Mkuu.

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu alisema kuwa jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali ni kusitisha shughuli za Mwenge na badala yake fedha hizo shilingi bilioni moja zimeelekezwa Wizara ya Afya ili kuwezesha shughuli mbalimbali zitakazosaidia kupambana na ugonjwa huo na tayari shilingi milioni 500 zimeshakabidhiwa Wizara ya Afya.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa angalizo kwa Wizara ya Afya na wafanyabiashara na kusisitiza: “Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kuthibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa viaa hivyo.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kufuatilia kwa karibu na kufanya uchunguzi kuhusu wageni watakao ingia katika maeneo, na wananchi wametakiwa kutoa taarifa katika namba za bure za 0800110037/0800110124 na 0800110125 pindi watakapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka.

Ugonjwa wa Corona ulioanza Disemba mwaka jana nchini China, umesambaa  zaidi katika nchi 150 duniani, na mgonjwa wa kwanza kugundulika nchini  ni Machi 16 mwaka huu ambaye aliwasili nchini kutoka Ubelgiji.

CORONA: TFF yasimamisha ligi zote
CORONA: EURO 2020 yapelekwa 2021