Kikosi cha Mtibwa Sugar kimeanza safari ya kurejea mkoani Morogoro kikitokea jijini Tanga, kufuatia mchezo wake dhidi ya Coastal Union uliokua umepangwa kuchezwa leo kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani kuahirishwa.

TFF jana ilitangaza kusimamisha michezo ya ligi zote, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Corona ambao umeingia nchini.

Mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema tayari kikosi chao kimeshaanza safari ya kuelekea Morogoro baada ya ligi kuu kusimamishwa.

“Tumepokea taarifa kuhusu kusimamishwa kwa Ligi Kuu Bara kutokana na kupambana na ugonjwa wa virusi vya Corona hivyo hatupingi tunatekeleza agizo bila hiyana na tunawaomba watanzania wachukue tahadhari,” amesema.

Michezo mingine ya ligi kuu ambayo ilitarajiwa kuchezwa leo jumatano Polisi Tanzania v Lipuli FC, Mbeya City v Alliance FC, JKT Tanzania v Singida United, Ndanda v Biashara United na Namungo v Kagera Sugar.

Ligi Kuu imesimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa alama zao 71, wakifuatiwa na Azam FC alama 54 baada ya wote kucheza michezo 28, wakati vigogo Young Africans ni wa tatu kwa alama zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za michezo 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC wenye alama 22 za michezo 28, Alliance FC alama 29, michezo 29, Mbeya City alama 30 michezo 29 na Ndanda FC alama 31 michezo 29.

Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar Juma Luizio Ndanda akiongea kuhusu umakini unastahili kuchukuliwa na watanzania, ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mgonjwa wa Corona aongea kwa mara ya kwanza "Naomba msamaha"
Euro milioni 150 kumng'oa Lautaro Martinez