Beki wa pembeni wa klabu ya Liverpool, Nathaniel Clyne amewataka wachezaji wenzake kuwa katika hali ya kujiamini wakati wote katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England dhidi ya Man Utd.

Clyne, aliyejiunga na Liverpool wakati wa majira ya kiangazi akitokea Southampton, ametoa rai hiyo kwa kutambua homa ya pambano kati ya majogoo wa jiji dhidi ya Man Utd ambayo huwa na viwango tofauti miongoni mwa wahusika wa pande zote mbili.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 24, amesema mchezo huo utakaochezwa mwishoni mwa juma hili utakua na mazingira magumu kutokana na matokeo mabovu yaliyowapata katika michezo iliyopita.

Amesema Man Utd watakua nyumbani Old Trafford wakitaka kuonyesha namna walivyojirekebisha kutokana na makossa waliyoyafanya ya kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Swansea City, ili hali kwa upande wao watahitaji kusaka ushindi ili kujiweka katika mipango mizuri ya kuendeleza ushindani kwenye msimamo wa ligi, baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya West Ham Utd kwa kufungwa mabao matatu kwa sifuri.

Hata hivyo Clyne amesisitiza kwamba upande wake yupo tayari kwa mpambano huo na hadhani kama kuna jambo lolote litakua kikwazo kwake kucheza kwa kujiamini na kufikia hatua ya kuisaidia Liverpool kufikia lengo la ushindi.

Amesema dhamira yake kubwa baada ya kujiunga na klabu hiyo ya Anfield ni kusaidiana na wenzake ili kufikia lengo linalokusudiwa huko Anfield na ana uhakika hata kwa wenzake hali ipo hivyo.

Kwa msimu uliopita Liverpool hawakufanya vizuri walipokutana na Man Utd katika michezo yao yote miwili ya ligi kuu soka nchini England baada ya kukubali kufungwa nyumbani na ugenini.

Azam FC Waweka Msimamo Kabla Ya VPL Kuanza
AS Roma Kusaidia Wimbi La Wahamiaji Barani Ulaya