Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) nchini wamelaani vikali vitendo vya ufukuaji makaburi ya watu wenye ulemavu huo na kuondoka na masalia ya viungo vinavyofanyika Mkoani Mbeya na maeneo mengine nchini vinavyofanywa na baadhi ya watu ambao bado wanaendekeza mila potofu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania, Nemes Temba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikiwaingiza kwenye hofu Kubwa na kukosa amani albino jambo ambalo linapingwa vikali huku wakiitaka serikali kuingilia kati ukomeshaji wa vitendo hivyo.

“Tunamuomba Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati suala hili, ikiwa ni kutumia nafasi yake kukemea uovu huu na kuwezesha kifedha mikakati iliyopo na itakayokuwepo yenye nia ya kukomesha uovu huu dhidi ya Watu Wenye Ualbino na zaidi jamii ipate hamasa na kuziacha fikra potofu na matendo ya kishirikina,” amesema Temba

Aidha, ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri na ya kupongezwa kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, hivyo wanamsihi, IGP Simon Sirro kuongeza kasi hasa katika upelelezi na kushiriki katika mchakato wa kuelimisha na kuhamasisha jamii kulinda na kuheshimu utu na uhuru wa Watu Wenye Ualbino na familia zao.

Tatizo watu wa Mbeya hawajazoea kuambiwa ukweli- RC Chalamila
Akothee anunua ugomvi wa Mange na Zari, ampasua Mange