Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kinatarajia kukutana na kuzungumza na Rais John Magufuli wiki ijayo, ambapo miongoni mwa mambo watakayomueleza ni changamoto za ukosefu wa ajira, udhalilishaji na motisha za watumishi.

Rais wa MAT Dkt Elisha Osati amesema kuwa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 mwezi huu, utashirikisha zaidi ya watumishi elfu moja wa kada ya afya.

“Tutanataka tumueleze Rais masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya afya, pamoja na kumpongeza kwa kazi kubwa iliyofanywa na serikali kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini,” amesema Dkt Osati.

Kuhusu tatizo la ajira kwa wahitimu dkt Osati amesema kuwa, kila mwaka wahitimu 1,500 wa taaluma ya udaktari wanaingia mtaani na hakuna ajira, lakini taarifa ya Wizara ya Afya inaeleza kuwa wana upungufu wa madaktari kwa asilimia 51.

Ameshauri kuwa ili kuweza kuondokana na hali hiyo, ni vema serikali ikashirikiana na sekta binafsi katika kujenga vituo vya afya nchini ili kusaidia kutoa ajira na huduma bora na za uhakika kwa wananchi.

Dkt Osati amesema kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO), daktari mmoja anapaswa kuhudumia watu elfu kumi kwa mwaka, lakini nchini Tanzania daktari mmoja anahudumia watu elfu 25 kwa mwaka.

RC Kilimanjaro azuia mshahara wa Mkurugenzi
Australia: Maafisa wafanikiwa kuzima moto wa muda mrefu