Chama Cha Demkokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka fumbo juu ya tuhuma za kuomba kura kanisani kwa misingi ya udini, zinazomkabili mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa.

Akizungumzia onyo lililotolewa na Mwenyekiti waTume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva dhidi ya kauli za Lowassa, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalim alisema kuwa bado chama chake hakijapata taarifa rasmi kutoka kwenye tume hiyo hivyo hawezi kuzungumzia lolote.

Jaji Lubuva alitoa onyo kwa vyama vya siasa vitakavyofanya kampeni kwa misingi ya udini na kueleza kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
“Tume haitasita kukifikisha chama cha mgombea mbele ya kamati ya maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake na atakaposhidnwa itaweza kutoa adhabu kali ikiwa ni pamoja na kukatazwa kuendelea na kampeni,” alisema Jaji Lubuva.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitoa tamko la chama chake na kulaani kitendo kilichofanywa na Lowassa huku akitaka wananchi kutomchagua kwa kuwa hana sifa za kuwa rais.

Akijibu hoja ya Nape, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema alisema kuwa hiyo ni kawaida ya CCM kuongea dhidi ya Chadema.

Hivi karibuni kilisambaa kipande cha video kinachomuonesha Edward Lowassa akiwa katika kanisa la KKT mkoani Tabora ambapo aliwaomba kura waumini wa kanisa hilo na kuwataka wamuombee zaidi kwa kuwa kwa mara ya kwanza rais anaweza kutoka katika kanisa hilo.

 

 

 

AS Roma Kusaidia Wimbi La Wahamiaji Barani Ulaya
Dk Slaa Afunguka Tena