Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kimesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi wilayani Bukoba mkoani Kagera, kwa kumshikilia na kumnyima dhamana Mwenyekiti wa Baraza la wanawake, Halima Mdee kitendo kinachodhaniwa kuwa ni cha kuendelea kuwanyanyasa na kuwakandamiza.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene ambapo amelitaka jeshi hilo kumtendea haki Halima Mdee kwa mujibu wa sheria, na kwamba wamuachie kwa dhamana, au wampeleke mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

”Polisi wanapaswa kumfanyia mambo matatu, kumuachia huru bila masharti, kama ana makosa wamuachie kwa dhamana kwa sababu kosa lake linadhaminika, au wampeleke Mahakamani akajibu tuhuma zake kama mashtaka yake yapo. kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria ni jambo ambalo halikubaliki”, amesema Makene.

Kwa upande wake Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya ameshangazwa na kitendo cha polisi kumkamata Halima Mdee, ilihali alikuwa anafanya kikao cha ndani cha wanawake, na kudai kuwa UWT wanafanya makongamano Kigoma.

Halima Mdee alikamatwa Julai 14, mara baada ya kumaliza kufanya kikao cha ndani cha kuwajengea uwezo wanawake wapya waliochaguliwa katika baraza hilo, anashikiliwa katika kituo cha Polisi Bukoba kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi.

Ndayiragije aonya kuhusu TP Mazembe
LIVE GEITA: Rais Magufuli akizindua Nyumba za Makazi ya Askari Polisi

Comments

comments