Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa msimamo wake dhidi ya vita ya maneno inayoendelea kati ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM), Humphrey Polepole imesema kuwa kauli ya Dkt. Bashiru kumtaka Membe ambaye ni mwanachama wa chama hicho kufika ofisini kwake ni ya kawaida ndani ya CCM.

“CCM inapenda kuwafahamisha kuwa imefuatilia kwa ukaribu mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wito alioutoa Dkt. Bashiru kwa Membe, Ni kama sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Katibu Mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM katika kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama,”imeeleza taarifa hiyo

Aidha, Chama hicho pia kimeelezea ushindi wake ilioupata katika uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye Kata 47 Tanzania Bara uliofanyika Desemba 2, 2018, ambapo CCM imepita bila kupingwa katika Kata 41 na katika Kata 6 ambako kumefanyika uchaguzi chama hicho kimeshinda kwa kishindo.

Hata hivyo, katika taarifa hiyo, Polepole ameongeza kuwa Desemba 17, chama kitakuwa na kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa huku Desemba 18, kitafanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa.

 

Rais Trump, mkewe watoa heshima zao za mwisho kwa Bush
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 4, 2018