Katika kuadhimisha sherehe ya miaka 42 tangu kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) February 05 mwaka 1977, viongozi wa chama hicho wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wameadhimisha siku hiyo kwa kupanda Miti ya Mbao na Matunda aina ya Parachichi katika kijiji cha Igodivaa kata ya Imalinyi.

Akitoa hotuba yake kwa wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo wilayani humo, mgeni rasmi Dkt. Susani Kolimba amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Igodivaa kwa kujitoa kushiriki katika ujenzi wa jengo lenye madarasa matatu katika Shule ya Msingi Igodivaa ambalo bado halijaezekwa huku akiahidi kuchangia baadhi ya vifaa kwa ajili ya kukamilisha Ujenzi huo.

Dkt. Kolimba ameahidi kupeleka vitabu 120 katika shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa kuanzia darasa la nne hadi darasa la saba vitabu ambavyo ameahidi kuukabidhi uongozi wa shule hiyo.

“Mimi ni Mwalimu nilipofika pale shuleni mwalimu mkuu aliniambia kuna uhaba wa vitabu vya darasa la tano mimi nikaona isiwe darasa la tano tu hapana sasa nitaleta vitabu 120 vya silabasi ambavyo vitakuwa vya kuanzia darasa la nne hadi darasa la saba ili ninapokuja kuwatembelea watoto wangu niwakute wanasoma namimi nitabarikiwa sana,”amesema Dkt. Kolimba

Aidha, katika hatua nyingine mbunge huyo wa viti maalum mkoa wa Njombe ametoa wito kwa wananchi wilayani Wanging’ombe na mkoa wa Njombe kwa ujumla kujiepusha na tabia za kujichukulia sheria mkononi juu ya matukio ya mauaji ya watoto yanayoendelea mkoani humo badala yake wananchi wafuate sheria pindi wanapohisi kuna mtu au watu wanaohusika na matukio hayo ya mauaji.

Hata hivyo, maadhimisho hayo pia yamehudhuliwa na baadhi ya viongozi wa CCM Mkoa wa Njombe akiwemo katibu Idara ya Umoja wa Wanawake Tanzania UWT mkoa wa Njombe, Anjela Milembe pamoja na mwenyekiti wa Idara ya vijana mkoani humo, Neemia Tweve.

Wasiochukua Vitambulisho Mtwara Watahadharishwa
Video: 27 wanaswa mauaji ya watoto Njombe, Mwanafunzi darasa la nne adaiwa kujinyonga

Comments

comments