Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Njombe kimepiga marufuku viongozi wa serikali mkoani humo kuchangisha michango wananchi isiyo na makubaliano maalumu na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuwaibia wananchi.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho mkoani humo, Erasto Ngole wakati akizungumza na jamii kupitia kipindi cha Redio kiitwacho Breakfast Club kinachorushwa Redio Kings Fm iliyopo Njombe mjini.

Amesema kuwa uongozi wa chama umeamua kutoa maagizo hayo kwa viongozi wa serikali kufuatia baadhi ya viongozi mjini Njombe kutoa maelekezo ya kuwataka wananchi (wazazi) katika shule ya Sekondari Maheve na Mabatini wachangie madawati pamoja na michango mbalimbali.

“Chama kinaelekeza kuwa viongozi wa serikali hasa sekta ya elimu wafuate utaratibu uliotolewa na Rais, tumeshangazwa na ujanja unaotumiwa na baadhi ya waratibu wa Elimu pamoja na walimu wakuu katika shule zetu,”amesema Ngole

Aidha, katika hatua nyingine uongozi wa CCM mkoani humo umempongeza Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri ambaye ameonyesha kupambana na kuwachukulia hatua viongozi wanaochangisha wazazi fedha za madawati.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya ya Njombe amemwagiza mkurugenzi kuwa waratibu elimu wa kata wote waliohusika kuwachangisha michango wazazi wachukuliwe hatua na hatua ikiwemo kuwapunguzia madaraka huku akizuia kuwahamisha akisema kuwa watahama na matatizo.

 

Kamati ya Maendeleo ya Kata yamgomea DC
Wafanyabiashara Dodoma hatarini kupata Magonjwa

Comments

comments