Licha ya kusikia kwenye mikutano kadhaa ya CCM kuwa wako tayari kushiriki katika mdahalo wa urais utakaoandaliwa na taasisi yoyote nchini, taarifa rasmi zinaeleza kuwa chama hicho kimekwepa kujibu barua rasmi ya uthibitisho wa ushiriki wao.

Kwa mujibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambalo lilipanga kufanya mdahalo wa urais September 10 mwaka huu, na tangu mwezi Agosti lilituma barua rasmi kwa vyama vyote vya siasa kutaka uthibitisho wa kushiriki kwenye mdahalo huo ambao ungewahusisha wagombea urais na wagombea wenza. Hata hivyo, hadi September 22 CCM na Chadema walikuwa hawajajibu barua hiyo.

“Mpaka sasa vyama vilivyothibitisha kushiriki ni viwili tu,Chaumma na TLP,” alisema Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alipoongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa ingawa CCM walisikika kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa wako tayari kushiriki mdahalo utakaowashirikisha wagombea urais, chama hicho hakijajibu barua hiyo rasmi ambayo ingeonesha uthibitisho wao rasmi wa kushiriki ili waandaaje wawe na uhakika na kufanya maandalizi kulingana na washiriki.

Mukajanga aliongeza kuwa hoja ya Chadema kutaka wenyeviti wa vyama kuwawakilisha wagombea urais kwenye mdahalo haikubaliki kwa kuwa mdahalo huo unalenga katika kuwahusisha wagombea urais na wagombea wenza na si vinginevyo.

Wajibu taarifa hizo, Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba na Mwenyekiti msaidizi wa chama hicho, Philip Mangula walitoa kauli ambazo zilionekana kutofautiana.

January Makamba alieleza kuwa walipokea barua hiyo na kuijibu September 13 na kwamba Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana alifanya vikao na maafisa wa MCT, wakati huohuo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho alieleza kuwa hajawahi kupata barua ya aina hiyo na kwamba angeipata angeifanyia kazi.

Hata hivyo, Septemba 13 ilikuwa siku tatu baada ya siku iliyokuwa imependekezwa kwa ajili ya mdahalo na MCT.

Awali, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliwataka CCM kushiriki katika mdahalo kwa kutuma wenyeviti wa vyama vyote. Wito huo ulijibiwa na CCM kupitia majukwaa ya kampeni na vyombo vya habari kuwa wako tayari kushiriki mdahalo lakini uwahusishe wagombea urais wenyewe.

 

CCM Yataja Idadi Ya Simu Alizonazo Magufuli Kama Sifa Ya Rais Anayefaa!
2Face Awasilisha Ombi Maalum Kwa Dbanj Na Donjazzy