Shirikisho la soka nchini Brazil CBF, limelilalamikia shirikisho la soka duniani FIFA kufuatia matumizi hafifu ya teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR), wakati wa mchezo wao wa kwanza katika fainali za kombe la dunia dhidi ya Uswiz uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.

CBF wamewasilisha malalamiko hayo FIFA, baada ya wachezaji wa kikosi cha timu yao ya taifa kumlalamikia mwamuzi kuhusu faulo aliyochezewa beki Miranda kabla ya Steven Zuber hajafunga bao la kusawazisha, siku ya jumapili.

CBF wameitaka FIFA kuwataka waamuzi kufuatilia matukio yanalolalamikiwa na wachezaji ili kujiridhisha kama yana ukweli, ili kuondoa utata ambao huenda ukawa chanzo cha upande mmoja kuhisi umeonewa kwa makusudi.

Tukio lingine lililolalamikiwa na CBF, ni lile la mshambuliaji Gabriel Jesus kuangushwa kwenye eneo la hatari la Uswiz, na mwamuzi aliliacha bila kuthibitisha kupitia teknologia hiyo ambayo tayari imeshatumika katika baadhi ya michezo na kutoa maamuzi.

” CBF imeitaka FIFA kuhakikisha teknolojia ya VAR inatumika ipasavyo, na sio tu mwamuzi anapotaka kufanya hivyo, wachezaji wanapolalamikia tukio lenye utata linapaswa kufuatiliwa na sio kuachwa.” Imeeleza taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya CBF.

Teknolojia ya VAR imeanza kutumika katika fainali za kombe la dunia mwaka huu, kwa lengo la kumaliza utata wa maamuzi ambayo katika fainali zilizopita yalizua tafrani na maneno mengi kutoka kwa wadau wa soka, huku wengine wakisema baadhi ya timu zilikua zikionewa kwa makusudi.

Mbowe aweka hadharani kinachomsumbua
Zaidi ya nusu ya bidhaa soko la Uganda ni ‘feki’