Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema kuwa amebaini kuwa kiasi cha Sh. 300 milioni zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Chama cha Wananchi (CUF) kwenda kwenye akaunti binafsi.

Alisema kiasi hicho ni sehemu ya Sh. 369.38 milioni ambazo chama hicho kilipewa kama ruzuku.

Aidha, alieleza kuwa chama hicho, bila kufuata utaratibu kiliondoa Saini ya Katibu Mkuu wa chama kwenye orodha ya watu wanaoidhinisha utoaji fedha kwenye akaunti za chama hicho.

Katika hatua nyingine, CAG pia alisema amebaini kuwepo kwa upungufu kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema chama hicho kilimtoa mpangaji kwenye jengo lake bila kuzingatia taratibu, hali iliyosababisha mpangaji huyo kufungua kesi na kudai Sh 800 milioni.

Alisema hata hivyo, CCM walizungumza na mlalamikaji na kufikia muafaka nje ya mahakama, ambapo walimlipa Sh. 60 milioni kama fidia.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti yake mbele ya Rais John Magufuli, leo, Machi 26, 2020 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, CAG alivitaka vyama vya siasa kuzingatia sheria na taratibu za fedha.

Magufuli ambana IGP " Serikali haiwezi kulipa mshahara waliokufa"
Magufuli asema Corona haitaahirisha uchaguzi mkuu 2020