Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema kuwa ukaguzi walioufanya umebaini kuwepo kwa malipo hewa yenye thamani ya mabilioni katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na malipo yaliyokuwa na shaka.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, CAG ameeleza kuwa katika ukaguzi maalum walioufanya, walibaini kuwa NHIF ilifanya malipo hewa ya Sh. 2.61 bilioni kwa mzabuni.

“Katika uchunguzi wetu wa vitabu vya fedha, taarifa za benki na hati za malipo za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya tulibaini kuwepo kwa malipo ya kiasi cha shilingi bilioni 3; kati ya malipo hayo Sh. 2.61 bilioni yalikuwa malipo hewa, Sh. 350.87 milioni ni malipo ambayo walipwaji walishindwa kubainika na Sh. 42.6 Milioni hazikuweza kuthibitika kupokelewa na walipwaji,” alisema CAG.

Alisema kuwa malipo ya Sh.42.6 milioni yalipaswa kulipwa kwa hundi iliyofungwa lakini yalifanywa kwa malipo ya fedha taslimu kinyume cha kanuni za fedha za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Katika hatua nyingine, CAG alieleza kuwa Shirika la Bima la Taifa (NIC) lilinunua mfumo usiofanya kazi kwa $3.59 Milioni. Alisema kuwa kutokana na manunuzi hayo, thamani ya fedha haikupatikana.

Aidha, CAG alieleza kuwa uchunguzi maalum ulibaini udanganyifu katika malipo yaliyofikia Sh. 267.89 milioni katika akaunti za matumizi mengine (OC), katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo. Alieleza kuwa walibaini baadhi ya watumishi walifanya malipo bila kuwa na viambatinishi husika lakini pia kwa malipo mengine viambatanishi vilivyokuwepo vilikuwa vinatia mashaka.

CAG ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia Ripoti yake inayohusu matumizi ya fedha ya hadi Juni, 2018

Rais Magufuli atoa siku 30 kituo cha mabasi Njombe kukamilika
Haya hapa makampuni 14 yaliyotajwa na CAG kuwa na hali mbaya kifedha