Wabunge nchini Uingereza wamepiga kura ya kuizuia nchi hiyo kuondoka katika Umoja wa Ulaya bila ya kufikiwa makubaliano ya aina yoyote kuhusu masuala mbalimbali.

Wabunge 321 wamepiga kura kupinga hatua hiyo, huku 278 wakiunga mkono Uingereza kuondoka kwenye umoja huo kiholela, ambapo kura ya jana imepigwa baada ya ile ya Jumanne, ambapo wabunge waliukataa mpango wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kuhusu masharti ya nchi hiyo kuachana na Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit.

Hatua ya Uingereza kuondoka bila ya makubaliano kuhusu uhusiano wa baadae kati ya pande hizo mbili, ungesababisha hatari kubwa katika biashara na mustakabali wa watu wa Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Kinachofuata kwasasa ni kura itakayopigwa hii leo na wabunge wa Uingereza kuamua iwapo wauombe Umoja wa Ulaya kuuchelewesha muda wa Brexit wa Machi 29, uliokuwa umepangwa awali kisheria. ambapo suala la kuongeza muda wa Brexit linahitaji kuidhinishwa na nchi zote 27 wanachana wa Umoja wa Ulaya.

Serikali ya Theresa May imesema kuwa itapendekeza kura ya tatu bungeni kuhusu mpango wa Brexit ifanyike Machi 20 kabla ya mkutano huo wa kilele, ambapo kama wabunge wa Uingereza wataukataa tena mpango huo, May amesema ataomba mchakato wa Brexit ucheleweshwe hadi Juni 30.

Aidha, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema kuwa ombi la kuchelewesha muda wa Brexit litafikiriwa, lakini sio moja kwa moja, ambapo amesema serikali ya Uingereza inahitaji kuueleza Umoja wa Ulaya kuhusu suala hilo na hasa kama litakuwa na mantiki.

Kwa upande wake Mwakilishi wa bunge la Umoja wa Ulaya anayesimamia mchakato wa Brexit, Guy Verhofstadt amesema kuwa anapinga hatua yoyote ya kuongeza muda wa Brexit, iwe ni kwa siku moja, wiki moja au hata saa 24, kama haitokani na kile kilichofikiwa na wabunge wa Uingereza, ameitaka serikali ya Uingereza kuamua kuhusu Brexit, kwa sababu hali ya kutokuwa na uhakika haiwezi kuendelea.

 

Trump azuia ndege za Boeing 737 MAX 8 kuruka anga la Marekani
Video: DC Kisare aupongeza mradi wa TACIP, awataka wasanii kuchangamkia fursa hiyo