Benki kuu ya Tanzania imepitisha ombi la kuunganishwa kwa benki za Twiga Bancorp (Twiga Bancorp Limited) na benki ya TPB (TPB Bank Plc) na kuwa benki moja kuanzia tarehe 17 Mei 2018 itakayoendelea kuitwa benki ya TPB (TPB Bank Plc).

Kufuatia hatua hiyo Wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote ya benki ya Twiga yatahamishiwa kwenda benki ya TPB.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 16, 2018 na Benki Kuu ya Tanzania chini ya Mamlaka iliyopewa ya kifungu cha 30(1)(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Ikumbukwe kuwa benki ya Twiga iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu kuanzia tarehe 28 Oktoba 2016 kutokana na kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji.

Hivyo, muungano huu utaifanya Benki Kuu kusitisha usimamizi wa benki ya Twiga na mambo yote kuhusiana na benki hiyo yatafanywa na benki ya TPB kuanzia tarehe 17 Mei 2018.

Benki mpya ya TPB itakuwa ina mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Uamuzi huu umechukuliwa ili kuboresha uangalizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

 

Dar24 inakusogeza karibu na Urusi, Kombe la Dunia 2018
Mmiliki wa lori lenye mizoga 12 atiwa mbaroni