Mwanafamilia wa kundi la Weusi, Bonta aka Maarifa amefunguka tena baada ya kuzua gumzo kwenye instagram alipouliza kuhusu matumizi ya wimbo wake ‘Tokomeza Zero’ kwenye kampeni inayoendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

Rapa huyo ameiambia A-FM ya jijini Dodoma kuwa alichohitaji yeye sio haki ya maneno ‘Tokomeza Zero’, bali ni haki ya wimbo wake ambao amedai umekuwa ukitumika kwenye kampeni hiyo bila kumhusisha yeye.

“Mimi sina tatizo na utumikaji wa neno ‘Tokemeza Ziro’, maneno haya wote tunazaliwa tunayakuta. Kila mtanzania ana haki ya kuyatumia aidha kwa kuyaimba au kwa kuyatamka,” Bonta ameiambia Mchaka Mchaka ya A-FM.

“Sasa mimi sina tatizo na neno ‘Tokomeza Ziro’, ila mimi tatizo langu ni kwamba kwenye ile kampeni iliyofanyika juzi ya Mheshimiwa DC wa Kisarawe, alikuwa anafanya matangazo ya ku-promote hiyo kampeni na yale matangazo yalikuwa yanaambatana na kutumika kwa wimbo wangu wa ‘Tokomeza Ziro’,”

“Hapo mimi ndipo nilipoeleza kwamba, kama wimbo wangu unatumika kwenye hii kampeni kuna heshima inabidi nipewe, kuna namna inabidi nitambuliwe la hasha basi ungetumika ule wimbo wa wasanii wengine, au wimbo mwingine wowote wenye maneno Tokomeza Ziro lakini sio ule wangu niliomshirikisha Baraka Da Prince,” alisema Bonta.

DC Jokate ameendesha kampeni iliyofanikiwa kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu wilayani kwake akichangisha michango kwa lengo la kuwasaidia watoto kwenye sekta ya elimu.

Bonta aliachia ‘Tokomeza Ziro’ mwaka mmoja uliopita akimshirikisha Baraka Da Prince, wimbo ambao ulipata nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari hasa wakati ambapo matokeo ya kidato cha nne yalitoka na kuwa gumzo.

Uchambuzi: ‘Leo’ ya Darassa na Jux ni moto wa gesi (Video)
Mwanamke aliyejifungua watoto watano ‘kwa mpigo’ afariki