Ulipaji wa fidia ya shilingi Bilioni 7 kwa wakazi 2,868 wa Vijiji viwili vya Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma kupisha ujenzi wa mradi wa maji bwawa la Farkwa, unatarajia kuanza Oktoba 10 hadi 31, 2019.

Hayo yamebainishwa hii leo na Mkuu wa Wilaya ya Chemba Simon Odunga na kuongeza kuwa fedha hizo zitalipwa kwa wananchi hao kwa kuhusisha taasisi mbalimbali kama makanisa, misikiti, ofisi za Vijiji na vyama vya siasa.

“Fidia hii ni kwa vijiji vya Bubutole na Mwambose na haitahusisha ofisi za Serikali kama vile Zahanati, miradi mbalimbali na shule, hasa itahusisha mali zote za wananchi na tutaanza kulipa kwani pesa tayari ipo tangu mwezi Agosti mwaka huu Wizarani,” amefafanua Odunga.

Amesema tayari Katibu mkuu wa wizara ya maji ameunda kikosi maalumu na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano ili zoezi la ulipaji wa fidia liweze kufanyika bila vikwazo na mradi huo unaopeleka maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Chemba, Bahi, Kondoa na Dodoma mjini uweze kuanza.

Kuhusu utaratibu wa uhamaji kwa wananchi wa vijiji hivyo mkuu huyo wa wilaya amesema watatakiwa kuhama ndani ya siku 90 baada ya kupokea malipo yao kama ambavyo sheria inavyoelekeza na kusisitiza wananchi juu ya kuheshimu maelekezo husika.

“Kiutaratibu wanapewa siku 90 tu za kuhama maeneo yao lakini hii inafanyika baada ya kupokea malipo hivi ndivyo sheria inaelekeza na baada ya hapo kama mtu anakiuka huwa kuna taratibu zingine za kufuata lakini ni matumaini yetu zoezi litaenda vizuri,” ameongeza

Makamu wa Rais atembelea shamba la miti, kampeni Dodoma ya kijani
TMA yataja Dar kupata mvua kubwa zaidi, yashauri