Jeshi la Polisi nchini Kenya linachunguza tukio la kubakwa na kuuawa kwa ajuza mwenye umri wa miaka 75 mkaazi wa Kijiji cha Kiandegwa, Kaunti ya Kirinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa za awali za jeshi hilo, ajuza huyo alitupwa kilometa kadhaa kutoka nyumbani kwake. Imeelezwa kuwa alikuwa peke yake nyumbani wakati ambapo wabakaji hao walipovamia na kutekeleza unyama dhidi yake.

“Tunasadiki kuwa mwanamke huyo alibakwa kabla ya kuuawa na mwili wake kutupwa mbali na nyumba yake,” alisema Chifu Geoffrey Mithamo, kiongozi wa eneo la Wamumu.

Kijana wa kiume wa bibi huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa walipewa taarifa na majirani na kwamba walishtushwa na taarifa hizo kwakuwa walikuwa wamezungumza na mama yao siku moja kabla.

“Tulishtushwa sana na taarifa hizo kwa sababu tulikuwa na mazungumzo marefu na yeye Jumapili majira ya saa nne usiku,” alisema kijana huyo.

Wapelelezi kutoka kituo cha polisi cha Sagana walifika katika eneo la tukio Jumatatu, majira ya saa sita na nusu mchana na walieleza kuwa marehemu alikuwa kwenye mapambano makali kabla ya kupoteza Maisha.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia miili kwenye hospitali ya Karira na upelelezi unaendelea.

Uchaguzi Serikali za Mitaa: Jafo aeleza siri ya CCM kushinda asilimia 99.7
RC akamata gari la kubeba maji likiwa limebeba wafanyakazi 30