Meneja wa klabu ya Real Madrid, Rafael Benitez amekataa kumjibu Jose Mourinho baada ya kurushiwa vijembe vilivyogusa maisha yake kisoka pamoja na familia yake.

Benitez, ambaye kwa sasa yupo mashariki ya mbali (China) sambamba na kikosi chake ambacho kinajiandaa na msimu mpya wa ligi, hakujibu jambo lolote pale alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya vijembe alivyorushiwa na Mourinho.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania, amesema yeye ni mwanasoka na katu hawezi kuyapa nafasi mazingira ya kipuuzi ambayo yamekua yakitengenezwa na watu wachache, kwa kujitafutia umaarufu duniani.

Amesema kwa sasa ni wakati mzuri kwake kuendelea na harakati za kukiandaa kikosi cha Real Madrid kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya AC Milan ambao utamsaidia kwenye mipango yake ya kufikia lengo la kufanya vyema msimu ujao wa ligi.

Chokochoko dhidi ya Benitez, zimechagizwa na kauli ya mke wa meneja huyo wa Real Madrid, Montserrat Seara, baada ya kusisitiza mara zote mume wake amekuwa akifanya vyema pale Mourinho alipopita huku akitolea mifano ya timu za Inter, Chelsea na sasa The Galacticos.

Kufuatia msisitizo huo Jose Mourinho hakuwa nyuma badala yake aliamua kurudisha mashambulizi kwa kusema maneno ya kashfa.

Mourinho aliwambia waandishi wa habari akiwa nchini Marekani kwamba, anahisi mke wa Benitez atakuwa amechanganyikiwa kwa namna fulani, kwa sababu mume wake alienda Chelsea kumrithi, Roberto Di Matteo na pia ameenda Real Madrid kumrithi Carlo Ancelotti.

Alisema kazi ambayo Benitez aliirithi kutoka kwake ni Inter Milan pekee, ambapo kwa takribani muda wa miezi sita tu alikiharibu kikosi ambacho kilikuwa bora barani Ulaya kwa kipindi hicho.

Mourinho aliongeza maneno yake kwa kumshauri mke wa Benitez kwa kumtaka aache kuzungumza kumuhusu yeye, kwani anahitaji kuutumia muda wake vizuri kufikiria diet (Mpangilio wa vyakula) ya mumuwe.

Rio de Janeiro Ina Kasoro, Michezo Ya Olympic 2016
Maradona Amtuhumu Mkewe Kumuibia Fedha Zake