Nchini Kenya maeneo ya Magharibi na Kati viwanda vya kusaga unga wa mahindi vimefungwa kutokana na ukosefu wa mahindi na hatua ya serikali kuchelewa kutoa magunia milioni 2 ili kukabiliana na makali ya njaa nchini humo.

Ambapo kwa sasa bei ya unga imepanda na kufanya gunia moja la kilo 90 lililokuwa likiuzwa kwa Sh2,600 sasa kuuzwa kwa Sh3,200 katika eneo la North Rift na kilo mbili za unga wa mahindi zinauzwa kati ya Sh115 na Sh130 ya Kenya ikilinganishwa na Sh80 bei iliyokuwa ikiuzwa wiki chache zilizopita.

Hadi sasa viwanda 10 vimefungwa kwa muda kati ya hivyo ni pamoja na Mombasa Millers, Unga, Pembe, Dolar na Kitui Millers ambapo wafanyakazi wameagizwa kwenda likizo ya lazima kutokana na ukosefu wa mahindi.

Baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi yametajwa kuwa ni  Bungoma, Busia, Kisumu, Narok, Kajiado na vingine vinne katika eneo la Kati.

“Hatujakuwa tukipata mahindi ya kutosha sasa tumeamua kufunga viwanda,” akasema msimamizi wa moja ya viwanda vilivyoathiriwa, na kuongezea kuwa asilimia 80 ya viwanda vimesitisha operesheni kutokana na uhaba wa mahindi.

“Viwanda vilivyoko katika maeneo ya Eldoret, Moi’s Bride na Kitale bado vingali na mahindi lakini yataisha ndani ya miezi miwili,” akasema Bw David Kosgei, msimamizi wa kiwanda cha nafaka mjini Eldoret.

Hata hivyo Serikali imeahidi kutoa magunia milioni mbili ili kukinga Wakenya dhidi ya bei ya unga wa mahindi ambayo inazidi kupanda, na watumiaji wamehimiza Serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru zaidi ya Wakenya milioni 22 na makali ya njaa.

“Waziri anafaa kujitokeza na kuwaeleza Wakenya kiasi cha mahindi yaliyosalia. Hatuwezi kuendelea na mchezo wa pata potea na maisha ya Wakenya,” akasema James Maina, mfanyabiashara mjini Eldoret.

Huku Serikali ikidai kuwa kwa sasa haitaagiza mahindi kutoka mataifa ya kigeni.

Nandy ufunguka ajali iliyowapata kuelekea Sumbawanga
Mlinzi aliye muua mwanafunzi ahukumiwa kunyongwa

Comments

comments