Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe amewaunga mkono Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kulaani tukio la kikatili lililomtokea Katibu wa CHADEMA Kata ya Hananasif, Daniel John siku za karibuni.

Bashe ametoa kauli hiyo katika jukwaa la CCM wakati akimuombea ridhaa mgombea wao Maulid Mtulia ili aweze kuwa muwakilishi wa Jimbo la Kinondoni katika siku zijazo endapo atapata kura nyingi za ndio siku ya kupiga kura.

“Naviomba vyombo vya ulinzi na usalama, vifanye kila jitihada kufanya uchunguzi wa kina ili aliyefanya uhalifu huu aweze kupatikana. Kumekuwa na tabia kila uchaguzi mdogo unapofanyika matendo ya kihalifu hufanyika halafu wenzetu wa upande wa pili huamishia kesi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM)”, amesema Bashe.

Pamoja na hayo, Bashe ameendelea kwa kusema “jambo hili lililotokea Jimbo la Kinondoni ni la kulaaniwa, sisi tunalilaani na nyie wananchi wa Kinondoni muendelee kulilaani lakini tuombe uchaguzi ufanyike na anayehusika apelekwe kwenye vyombo vya dola, ashtakiwe na watanzania tuambiwe ni nani anayehusika na tukio hili”.

Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi Kinondoni Murilo Jumanne Murilo amesema Jeshi lake litachunguza kifo cha Kiongozi wa CHADEMA kata ya Hananasif, ambaye mwili wake uliokotwa ukiwa na majeraha kwa kufuata misingi ya kazi yao na siyo kusukumwa na hisia za mtu binafsi.

Waziri Mkuu wa Ethiopia ajiuzulu
Video: "Nakufahamu wewe ni mpole, nakuomba ukaze kidogo sauti" - Mwakibolwa