Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) ambalo jana liliibua gumzo mtandaoni baada ya kuweka wazi kuwa kanuni mpya yenye tozo mbalimbali kwenye kiwanda cha sanaa nchini itaanza kutumika Julai Mosi mwaka huu, wametetea uamuzi huo.

Baraza hilo lililazimika kutoa ufafanuzi kuhusu kanuni hizo ambazo zililalamikiwa na wasanii wengi baada ya kupata taarifa hizo, hususan kuhusu tozo ya Sh5 milioni kwa kampuni itakayomtumia msanii kutangaza biashara (branding) na Sh2 milioni kama malipo ya kuandaa tamasha.

Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa kanuni zilizopitishwa ambazo wadau wa muziki ikiwa ni pamoja na wasanii walishirikishwa.

Aidha, tofauti na kilio cha wasanii na wadau wa muziki kilichorindima jana kwenye mitandao ya kijamii, Mngereza amesema kanuni mpya zimelenga katika kusaidia sanaa nchini, kwani fedha zitakazokusanywa ni kwa manufaa ya wasanii na wadau wa sanaa.

Fedha hizo kwa mujibu wa Kanuni hizo mpya, zinazoonekana kwenye kifungu cha 15 cha kanuni hizo pamoja na Jedwali lake, zitakuwa pato la Basata.

“Tunalenga sana sana namna gani wasanii waingie mkataba, kwahiyo mkataba ndio utakaoonyesha kuwa kampuni hiyo inatakiwa ilipe milioni tano. Ni fedha ambazo kimsingi zinaingia kwenye mfumo wa kisheria na kikanuni kwa masuala ya kifedha,” alisema.

“Kwahiyo haina maana kwamba itamlipa msanii, ni shughuli kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya sanaa kwa manufaa ya wasanii na wadau wa sanaa,” aliongeza Mngereza.

Hata hivyo, ufafanuzi huo wa Basata huenda usitibu taharuki na mshtuko uliowakumba wasanii ambao wametumia mtandao wa Twitter kupinga tozo hizo wakidai kuwa zinaenda kuwaumiza.

Mtayarishaji wa mkongwa wa muziki, Paul Mathysse maarufu kama P-Funk Majani amewataka Basata kurudi kwa wadau na kufanya marekebisho ya tozo.

Majani amesema kuwa kipengele cha kumsajili msanii ni rafiki kwa msanii kwani kinamfanya atambulike na kufanya biashara, lakini malipo ya Sh5 milioni yanatakiwa kulipwa na kampuni inayomhitaji kufanya naye biashara pamoja na Sh2 milioni kwa kuandaa tamasha ni pigo.

P-Funk Majani

Akifafanua kile kilichosemwa na Majani, Nikki wa Pili  ambaye ni mwanahisa wa kampuni ya Weusi aliandika, “Katika biashara ya matangazo, kampuni ikitaka kufanya kazi na mimi itoe milioni 5 na mimi inilipe. Huoni kwamba hiyo kampuni itamchukua mtu mwingine wa kawaida, maana yake chanzo kingine cha mapato kimefungwa.”

“Hivi sasa tuna biashara mbili, sisi wenyewe kuandaa shows (maonesho) na pia biashara ya matangazo…. Hivi sasa kuandaa tamasha kibali ni milioni mbili, kibali cha ukumbi milioni moja, na bado tiketi kukatwa kodi, hata hatutaweza,”Nikki aliongeza.

Kwa mujibu wa tangazo la Basata, sheria imeanza kufanya kazi tangu Julai Mosi, hivyo leo ikiwa ni Julai 13 waliofanya kinyume wanavunja sheria.

Kama ilivyo kwa wamiliki wa vyombo vya habari mitandaoni waliotakiwa kujisajili na kulipia kupata leseni ili kutambulika, wasanii pia watalipa kiasi cha kati ya Sh15,000 hadi Sh50,000 kwa ajili ya usajili, hatua iliyoungwa mkono na baadhi ya wadau akiwemo P- Funk Majani.

Video: Kiongozi NCCR Mageuzi akimbilia CCM, afunguka madudu ya upinzani
Hii ndio sababu Diamond kufanya kama Shahrukh Khan video ya 'Baila'