Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limekanusha taarifa za kuwaruhusu wasanii wa lebo ya Wasafi, Diamond Platinumz na Ray Vanny kufanya tamasha nchini Kenya.

Kupitia barua yao iliyotolewa jana, Baraza hilo limesisitiza kuwa halijabadili uamuzi wa kuwafungia wasanii hao kufanya tamasha lolote ndani na nje ya nchi kwa kipindi kisichojulikana.

“Baraza kwa mara nyingine linawataka wasanii hao kutii maagizo waliyopewa na kuacha mara moja kupotosha umma kwa kusambaza taarifa za uongo kabla hatua kali zaidi kuchuliwa dhidi yao,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Onesmo Kayanda kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Basata.

Taarifa hiyo ya Basata imekuja saa chache baada ya Diamond kuandika kwenye Instagram ujumbe mrefu akiishukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo pamoja na Basata. Ujumbe huo ulitoa picha kuwa huenda Serikali imekubali kuwasamehe.

Lakini kutokana na taarifa ya Basata, Diamond bado haruhusiwi kufanya tamasha lake nchini Kenya kama alivyokuwa amepanga kufanya jijini Mombasa kwenye mkesha wa Krismasi.

Baraza hilo limewafungia Diamond na Ray Vanny kwa kipindi kisichojulikana kwa kuimba kwa makusudi wimbo wa Mwanza/Nyegezi ambao umefungiwa. Kadhalika, Baraza hilo limelifungia tamasha la Wasafi kwa kukiuka masharti ya kibali chake.

 

Video: UVCCM Kigoma wamvaa Zitto, 'Sio raia wa Tanzania
Juventus waweka tena mtego kumnasa Pogba