Mkazi wa Kijiji cha Kowak, Wilayani Rorya mkoani Mara, Juma Olemo, amekutwa amejinyonga hadi kufa katika Nyumba ya kulala wageni ya Silent Inn iliyopo mjini Tarime na kuacha ujumbe wa barua yanye kurasa mbili, akiwataka rafiki zake kuachana na waganga wa kienyeji wapotoshaji.

Akisoma ujumbe ulioandikwa katika barua hiyo kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Tarime – Rorya, Henry Mwaibambe, amesema Olemo aliomba msamaha kwa uamuzi aliouchukua na kuwaasha vijana wenzake kuachana na waganga wa kienyeji ambao wanawaaminisha kubadili maisha yao kwa imani za kishirikina.

Kamanda Mwaibambe amesema katika barua hiyo Olemo aliwataka marafiki na vijana wenzake, siku ya mazishi yake wacheze mpira wa miguu ili kumuaga.

” Novemba 7, mwaka huu, wahudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Silent Inn iliyopo mjini Tarime, baada ya kuamka asubuhi na kutaka kufanya usafi vymbani, walijaribu kugonga mlango wa chumba alimokuwa amelala Olemo lakini haukufunguliwa na kuwalazimu kuita askari polisi ili kushirikiana nao kufungua mlango huo” Amesema Kamanda Mwaibambe.

“Walifanikiwa kuvunja na walipoingia ndani walikuta mwili wa Olemo ukining’inia juu ya dari na pembeni yake walikuta barua hiyo iliyokuwa na ujumbe mrefu wa kurasa mbili” alieleza.

Na kuongeza kuwa ” Jamaa wa marehemu walifika na kubaini kuwa mwandiko uliomo kwenye barua hiyo ni wake marehemu ambapo katika ujumbe huo alimtaja mke wake na kuomba msamaha kwa uamuzi aliochukua na kumuomba ndugu yake mdogo kumtunza mkewake na watoto wake”

Pia aliwaomba msamaha mashabiki wa timu ya mpira Simba, kwa uamuzi wake wa kujinyonga, aliwaomba masamaha waendesha bodaboda na kuwaasa kufanya kazi halali na kutowaamini waganga wa kienyeji.

Kamanda amesema Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime na kufanyiwa uchunguzi kisha kuchukuliwa na ndugu zake kwa mazishi.

Wasomi kukosa ajira kwatajwa kuondoa utulivu wa kisiasa
Alexandre Lacazette awashauri wachezaji wa Arsenal