Viongozi wa taasisi za dini ya Kiislamu Mkoani Kagera wameaswa kuacha tofauti zao na kujiunga kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo ya waumini wa dini hiyo pamoja na jamii inayowazunguka kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Sheikhe wa Mkoa Kagera, Alhaji Kharuna Kichwabuta katika hafla ya uzinduzi wa mpango mkakati wa maendeleo wa miaka mitano ulioandaliwa na Taasisi ya Bakwata mkoa Kagera wenye kaulimbiu isemayo ‘Bakwata Mpya Kagera, Nguvu Moja kwa Pamoja’

Amesema kuwa katika kuujenga na kuutetea Uislamu, Waislamu wenyewe wanatakiwa kuwa wamoja na kuutanguliza Uislamu wao kwanza kabla ya mambo mengine ambapo amewaomba viongozi wa taasisi nyingine kuunga mkono mpango.

Kwa upande wake mjumbe wa baraza la maulamaa Taifa, Sheikhe Ally Mgeliko ambaye amesema kuwa mpango huo unalenga hasa huduma za kijamii zikiwemo shule huduma za afya na mambo mengine hivyo waislamu wanatakiwa kuu nga mkono kwa hali na mali.

Naye Mgeni rasimi katika hafla hiyo Brigedia Jenerali, Marco Gaguti ambaye ni mkuu wa mkoa Kagera amesema kuwa ofisi yake ipo wazi muda wote kwaajili yakuwahudumia waislamu na jamii nzima na kuahidi kuwa mpango huo sio wa Bakwata bali ni wa Wanakagera wote.

Aidha, Gaguti ameongeza kuwa ili mkoa wa Kagera uwe na amani, viongozi wa dini wanatakiwa kuhubiri suala la amani katika maeneo yao ili kuwajengea waumini wao kuwa na hofu ya mungu.

Wakazi wa Makete watakiwa kuchangamkia fursa za Uwekezaji
Pinda awafunda Watumishi Ofisi ya Waziri Mkuu