Mzuka wa Vanessa Mdee ulioifanya Tanzania kuwa katika kilele cha mauzo ya albam kali kwenye mtandao wa ‘Boomplay’ umehamia kwa mwimbaji mwingine wa kike, Nandy.

Nandy ametangaza ujio wa albam yake mpya na ya kwanza katika maisha yake aliyoibatiza jina la ‘The African Princess’, itakayoachiwa rasmi Novemba 11 mwaka huu.

Mkali huyo wa ‘Ninogeshe’ amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kupokea mzigo wa maana kutoka kwake, huku akiwapa njia ya kuweka oda (pre-order) mapema ili wawe wa kwanza kuipata.

Utaratibu huo wa Nandy unazifuata nyayo za Vee Money alipokuwa akitoa Money Mondays mwishoni mwa mwaka jana, ambapo albam yake ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye mauzo ya Boom Play Afrika Mashariki.

Kuna kila dalili kuwa ‘The African Princess’ pia inaweza kupata mapokeo ya maana, lakini tu kama utambulisho wake utafuata njia nzuri na sahihi za kiubunifu kama ilivyokuwa kwa ‘Money Mondays’.

Uzito na utamu wa Money Mondays nao ulisaidia kuisogeza kwa nguvu kwani kila aliyeigusa alimwambia na rafiki. Kuna dalili nzuri pia kwa Nandy kwani ngoma ambazo tayari zimetoka ni kubwa tayari, tunasubiri zile ambazo zitaingia ndani.

Ikumbukwe kuwa Nandy ana ahadi ya kufanya wimbo na Yemi Alade wa Nigeria ambaye alikubali uwezo wake, kuna kolabo nyingine amewahi kusikika akisema atafanya na msanii mmoja mkubwa wa kike wa Marekani… yote haya yanaweza kuwa dalili za kuinogesha ‘The African Princess’.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 21, 2018
Video: Ndege inayotumiwa na Rais wa Marekani katika ziara zake, ni ndege yenye ulinzi mkali haijawahi kutokea

Comments

comments