Kikosi cha Azam FC kimerejea jijini Dar es Salaam leo asubuhi tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Kikosi hicho kinatokea mjini Morogoro baada ya kuendeleza dozi nene kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa kuichapa Shupavu mabao 5-0, mchezo uliopigwa jana Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Hii ni mara ya pili inaibuka na ushindi mnono kwenye michuano hiyo baada ya mechi ya awali kuichapa Area C United ya Dodoma mabao 4-0.

Mshambuliaji kinda Paul Peter, alijiandikia rekodi ya aina yake tangu apandishwe kutoka timu ya vijana kwa kufunga hat-trick yake ya kwanza iliyochagiza ushindi huo mnono wa Azam FC.

Mbali na Peter, pia kulikuwa na kiwango kizuri kwa wachezaji wa Azam FC akiwemo winga Idd Kipagwile, mshambuliaji Yahya Zayd, Frank Domayo, mabeki Abdallah Kheri, David Mwantika na kipa Mwadini Ally, ambao waliukosa mchezo uliopita.

Bao la kwanza la Azam FC limeweka kimiani na Yahya Zayd dakika ya 44 kwa mkwaju wa penalti baada ya winga Idd Kipagwile, kuangushwa ndani ya eneo la 18.

Kipagwile akaipeleka mapumziko Azam FC kwa uongozi wa mabao 2-0, baada ya kutupia bao safi la pili akimtesa vilivyo kipa wa Shupavu.

Kipindi cha pili Azam FC iliongeza nguvu kwenye ushambuliaji kwa kumpumzisha Mbaraka Yusuph na kuingia Peter aliyemalizia mabao matatu ya nguvu dakika ya 56, 77 na 87.

Kwa matokeo hayo, Azam FC imesonga mbele kwa raundi ya 16 bora na kwa sasa inasubiria kupangiwa mpinzani wake.

Aymeric Laporte avunja rekodi Man City
Trump aendelea kusisitiza maslahi ya Marekani kwanza