Baada ya kufanikisha mchakato wa kumsajili mshambuliaji Bernard Arthur kutoka nchini Ghana, hatimaye uongozi wa Azam FC umetangaza hautofanya usajili mwingine katika kipindi hiki cha dirisha dogo.

Afisa Habari wa Azam FC, Jaffary Iddy Maganga ametangaza uamuzi huo leo Jumatano alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, ambapo amesisitiza  hawana mpango wa kusajili mchezaji mwingine katika kipindi.

Amesema usajili wa mshambuliaji huyo kutoka nchini Ghana umeziba pengo la mshambuliaji alieondoka Azam Complex majuma kadhaa yaliyopita Yahya Mohamed, baada ya kuafiki makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba wake, kutokana na kiwango chake kuwa duni.

“Kwa sasa tumefunga usajili kwenye kikosi chetu, hatutasajili tena mchezaji mwingine kwa sababu nafasi zimejaa, na hivi karibuni tulimuongezea mkataba kiungo wetu, Steven Kingue Mpondo raia wa Cameroon, kwa mahitaji ya benchi la ufundi kila kitu kimetimia kipindi hiki.” alisema Jaffary Iddy

Azam FC inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanznaia bara  ikiwa na pointi 23 sawa na Simba lakini imezidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, timu zote katika ligi hiyo zimeshacheza michezo 11 katika msimu huu wa 2017/18.

Young Africans waanza kujiandaa kisaikolojia
Kilimanjaro stars yaongeza watatu, kulifuata kombe la Chalenji kesho