Waimbaji wengi wakubwa Tanzania wamekuwa na historia ya kuanza muziki kwa kurap aka kufokafoka kabla hawajagundua kuwa sauti yao ni ‘lulu’ na biashara kubwa wakiamua kuimba.

Kwa kusikiliza sauti na ufundi mkubwa wa kuimba alionao boss wa Top Band, T.I.D, ni vigumu kugundua kuwa jamaa alikuwa rapa anaejiamini na hakuwa na mpango wa kuimba hata kidogo kabla ya kushikwa bega na AY aliyemuonesha upande sahihi anaotakiwa kuelekeza nguvu zake ili atusue.

Akiongea katika kipindi cha Chill na Sky kinachotayarishwa na skywalker, AY alisema kuwa alikuwa anamsikiliza T.I.D katika kazi zake za u-MC ambapo kwa mbwembwe za u-MC, T.I.D alipenda kuchombeza wimbo wa KC na Jojo ‘I’m missing You’.

Sauti yake iliyakuna masikio ya AY ambaye alikuwa na wimbo wa rap katika studio za MJ, wimbo aliouandika miaka mingi iliyopita akiwa na rafiki zake aliosoma nao kitambo, Buff G na Snare uliohitaji chorus ya kuimba. “Nilikuwa kila ninimsikiliza nasema ‘huyu jamaa anajua kuimba,” alisema AY.

Kwa umakini mkubwa, AY alimfanyia usaili T.I.D kadri alivyokuwa anaimba na akagundua kabisa kuwa ilikuwa sauti sahihi ya kunogesha kiitikio cha wimbo wao wa mapenzi walioubatiza jina la ‘My Girlfriend’.

Hata hivyo, ilimbidi AY amshawishi T.I.D kuachana na mpango wa kurap ili aimbe kwenye wimbo huo. Haikuwa rahisi, T.I.D aliweka vikwazo na ubishi kuwa yeye anataka kurap na sio kuimba, lakini mwisho wa siku alikubali kwenda kwa Master Jay, producer ambaye hakuukubali kwa haraka uwezo wake.

“Nilienda nae kwa Master J, Master J alikuwa hamtaki kabisa anasema ‘aah huyu aendelee kurap tu’. Akawa anapiga hadi pushap..! T.I.D mwenyewe alikuwa hataki [kuimba], anakwambia ‘hapana mimi nataka kuchana’. Nikamwambia T.I.D hebu imba…”AY alisimulia.

Baada ya ushawishi wa muda, Master Jay alimruhusu T.I.D kuingia booth na kufanya alichofanya, matokeo yalikuwa tofauti na walivyotarajia, chorus yake iliongeza utamu na ukubwa wa wimbo huo ambao baadae uliteka airwaves.

“Cheki alivyokamua humo ndani, alikamua vizuri sana,” Alisema AY. “Production ilikuwa ya John Mahundi na tulikuwa na Snare na Buff G, na ni wimbo ambao tuliuandika kitambo, tukiwa shule boarding [Ifunda Tech] zamani , 1997.”

Asante kwa AY, Mungu alimtumia kumuonesha TID miaka ile, na ameendelea kuwa msaada kwa wasanii wengi wa Tanzania hadi leo kwa kuwaonesha njia ya kuelekea anga za kimataifa, akiwemo Diamond Platinumz ambaye sasa ni moja kati ya wasanii wakubwa Afrika.

Chuba Akpom Amkuna Arsene Wenger
Forbes: Real Madrid Bado Tishio Kwa Utajiri Duniani