Mkazi wa Kijiji cha Isongole wilayani Ileje mkoani Songwe, Joseph Chomo (55) ameuawa kwa kupigwa na mkewe pamoja na watoto akidaiwa kuoa mke wa pili bila kuwashirikisha.

Hayo yamethibitishwa na mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude ambapo amesema kuwa tukio hilo lilitokea saa sita usiku wa kuamkia jana huku akibainisha kwamba chanzo halisi kinaendelea kuchunguzwa ili kubaini ukweli.

Amesema kuwa hadi jana mke na watoto wawili wa Chomo walikuwa wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumzia mkasa huo, mkazi wa kijiji hicho, Elifa Kalago amesema kuwa usiku huo walisikia sauti ya Chomo akiomba msaada na walipofika nyumbani kwake walimkuta amelala mlangoni huku akitokwa damu nyingi.

Aidha, ameongeza kuwa baada ya kuwauliza sababu ya tukio hilo hawakutoa jibu, ndipo walipoamua kumpeleka Chomo hospitali, lakini alipoteza maisha wakiwa njiani.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Ikomba Kayuni amesema kuwa wanafamilia hao walikuwa na ugomvi wa siku nyingi na ulianza baada ya baba mwenye nyumba kuoa mke wa pili bila kuwashirikisha, japokuwa awali ugomvi huo ulionekana kuisha.

Hata hivyo, hilo ni tukio la pili katika kipindi cha wiki mbili kutokea mkoani Songwe, ambapo mwishoni mwa mwezi uliopita mkazi wa Kijiji cha Bupigu wilayani Ileje alifariki dunia baada ya kupigwa na mkewe kutokana na wivu wa mapenzi

Amaber Ruth alimwa barua na BASATA
Ijue faida ya bamia katika mwili na ngozi yako