Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (AU), Dkt. Amina Mohammed (pichani) ameisihi Tanzania kuendelea kuimarisha amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na kuendelea kutoa askari wake kuungana na vikosi vya ulinzi wa amani duniani.

Dkt. Mohammed ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi Jijini New York nchini Marekani.

Amesema Umoja wa Mataifa unatambua mchango wa Tanzania katika ulinzi wa amani duniani na kwamba uko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza jitihada hizo ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama zaidi ya kuishi.

“Tanzania imekuwa muhimili muhimu katika kuhimiza amani katika ukanda wa maziwa makuu ikiwa ni pamoja na kuhifadhi wakimbizi kutoka ukanda huo kwa miaka mingi bila kuchoka,” alisema Dkt. Mohammed.

Kwa upande wa Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania inatambua nafasi ya Umoja wa Mataifa na kwamba itasalia kuwa mwanachama wa umoja huo.

“Napenda kukuhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kutoa askari wake katika vikosi vya ulinzi wa amani katika maeneo mbalimbali duniani,” alisema Prof. Kabudi

Waziri Kabudi alieleza hatua mbalimbali ambazo Tanzania imepiga katika masuala ya maendeleo endelevu (SDGs) ikiwa ni pamoja na afya, maji, ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi pamoja na masuala ya kuimarika kwa demokrasia nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Amina Mohammed na baadhi ya wajumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na wajumbe wake katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo New York Marekani

Prof. Kabudi amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Marekani alipokuwa akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Shule yafungwa baada ya kuzuka ugonjwa usioeleweka, wagonjwa watengwa
Uchafu wa vikombe chanzo cha kukatika umeme Dar, mtumishi atumbuliwa