Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa ‘Stiegler’s Gorge’ utaogharamu takribani Sh 6.5 Trilioni.

Gwajima amesema Rais Magufuli amefanya jambo zuri la kufanya Tanzania iwe na umeme wa kutosha utaowezesha kuendesha baadhi ya shughuli ikiwemo treni ya umeme.

Hayo amezungumza leo, Juni 3, 2019 alipomtembelea Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo ameongeza kuwa  umeme huu utakaozalishwa awamu hii ni mkubwa kuliko uliowahi kuzalishwa tangu kuundwa kwa Tanzania.

Akizungumzia pingamizi la wana mazingira kuhusu mradi huo, Askofu huyo alieleza kuwa ili upate faida ya umeme huo ni lazima kuwe na madhara kama mtu anavyopaswa kuvunja mayai yake ili apate chips kuku.

”Ili ule chips mayai lazima uvunje baadhi ya mayai, mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais hasa kwa juhudi zake za Stiegler’s Gorge mahala ambapo tutazalisha umeme mwingi kuliko tuliowahi kuzalisha hapo zamani.  Kumbuka wakati wa mwalimu Nyerere tulizalisha umeme kiasi wakati wa Mwinyi, wakati wa Mkapa, wakati wa Kikwete  lakini kupitia Stiegler’s Gorge tutazalisha umeme mwingi kuliko hata tulipoanza,” amesema Askofu Gwajima.

Alisema kuwa hata Marekani waliwahi kukataa kusaini makubaliano ya kimataifa ya mazingira yaliyowataka kupunguza idadi ya viwanda ili kusaidia kupunguza taka-moshi zitokanazo na viwanda na makaa ya mawe.

Aliongeza kuwa hapa tulipo hapajali sana kulinganisha na tunapokwenda kwani serikali inafanya kazi nzuri kwa makini na nidhamu kubwa.

Stiegler’s Gorge ni mradi mkubwa wa uzalishaji umeme kutoka mto Rufiji ambao utazalisha Megawati 2,100. Ujenzi wa mradi huo wa umeme utasababisha miti takribani milioni 2, hali inayoibua mvutano kwa wanamazingira hasa wa Magharibi.

Davido, Cardi B walivyokiamsha stage ya HOT 97
Athari za kiatu kirefu kwa mwanamke mjamzito

Comments

comments