Nchini Tanzania imebainika kuwa chanzo kikuu cha ajali za barabarani hususani kwa waendesha bodaboda ni makosa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na ulevi na uzembe ambao huchangia kwa asilimia 76 ya ajali zote.

Hayo yamebainishwa na naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Masauni, leo katika vikao vya bunge vinavyoendelea Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo aliyehoji licha ya kazi nzuri ya waendesha bodaboda ya kurahisisha usafiri na kupunguza tatizo la ajira, bado zipo changamoto kama ajali za mara kwa mara pamoja na wizi, nini mkakati wa serikali kupunguza tatizo hilo

Mhandisi Masauni amesema kuwa vipo vyanzo vikuu vitatu vinavyosababisha ajali za barabarani hapa nchini ikiwa ni pamoja na makosa ya kibinadamu ambayo huchangia kwa asilimia 76, ubovu wa magari asilimia 16 na mazingira ya  barabara asilimi 8.

Pia ameyataja baadhi ya makosa ya kibinadamu ni pamoja na ulevi, uendeshaji wa kizembe, mwendokasi, uzembe wa waendesha pikipiki, baiskeli na uzembe wa watembea kwa miguu.

Aidha amesema kuwa Serikali kupitia jeshi la polisi hapa nchini wamekuwa wakitoa elimu kwa waendesha bodaboda namna nzuri ya utumiaji wa pikipiki ikiwa ni pamoja na kuvaa kofia ngumu, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa leseni kwa waendesha bodaboda ili kupunguza waendeshaji wasio na leseni na wanaoweza kusababisha ajali.

Video: Vinyozi na Wasusi: Tunatumia ujanja | Elimu ya nini? | Kuna magonjwa | TACIP kuwasajili
Hakuna mtu atakayekamatwa kwa kukutwa na vifungashio- Makamba