Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Tanzania bara (ASFC) Azam FC wataendelea na mpango wa kutetea taji hiyo mbele ya Simba SC kwenye mchezo wa Robo Fainali utakaochezwa jijini Dar es salaam mwezi ujao.

Wawili hao wamepangwa kukutana katika hatua ya robo fainali, baada ya Shirikisho la soka nchini TFF kuendesha Droo ya Robo Fainali leo asubuhi kwenye Studio za Azam TV na kuratibiwa na meneja mashindano wa Shirikisho hilo Baraka Kizuguto.

Michezo mingine ya Robo Fainali iliyofahamika baada ya Droo hiyo, Kagera Sugar iliyo chini ya kocha mzawa Mecky Maxime  itamenyana na Young Aficans inayonolewa na kocha wa kigeni Luc Eymael.

Alliance FC kutoka jijini Mwanza itamenyana na Namungo FC ya mkoani Lindi huku Sahare All Stars ambayo ni timu pekee inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kutinga hatua ya robo fainali itamenyana na Ndanda FC ya mkoani Mtwara.

Mbali na michezo ya robo fainali kupangwa, pia droo hiyo ilimaliza ubishi kwa hatua ya nusu fainali kuanikwa.

Mshindi wa mchezo kati ya Simba SC na Azam FC atakutana na mshindi kati ya mchezo wa Young Africans na Kagera Sugar, hivyo ili hawa watani wajadi wakutane ni lazima kila mmoja ashinde mchezo wake ili wakutane hatua ya nusu fainali.

Kwa upande wa mshindi wa Alliance FC na Namungo FC atakutana na mshindi wa mchezo kati ya Ndanda FC dhidi ya Sahare All Stars.

CAF kunusuru uchumi wa soka la Afrika
Tetesi za usajili barani Ulaya