Aliyekua meneja wa klabu ya Arsenal ya England Arsene Wenger, amekanusha taarifa za kuzungumza na mwenyekiti wa FC Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge, kwa ajili ya kumuomba kazi.

Wenger amekanusha taarifa hizo, baada ya jarida la Bild la Ujerumani kuthibitisha kulikuwepo na mazungumzo baina ya pande hizo mbili, juzi Jumatano.

Meneja huyo kutoka nchini Ufaransa amesema hakuwahi na wala hatowahi kufanya mazungumzo ya kuomba kazi kwenye klabu yoyote, zaidi ya kusubiri ofa, kama ilivyo taratibu za mchezo wa soka.

FC Bayern Munich wapo kwenye mchakato wa kumsaka meneja mpya, kufuatia kumtimua Niko Kovac, baada ya kikosi chao kufungwa mabao matano kwa moja dhidi ya Eintracht Frankfurt, siku ya Jumamosi.

Wenger ana rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi ya England mara tatu kombe la FA mara saba, katika kipindi cha ukufunzi wake wa miaka 22 akiwa na kikosi cha Arsenal, kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu wa 2017-18.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 70, kwa sasa anafanya shughuli za uchambuzi wa soka kwenye televisheni ya beIN Sports, na aliitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa za kuomba kazi FC Bayern Munich.

“Niliwahi kukaribia kujiunga na Bayern miaka kadhaa iliyopita, lakini sikufanya hivyo kwa sababu nilikua na majukumu mazito nikiwa na Arsenal, sijawahi na wala sitowahi kuomba nafasi ya kazi kama ilivyoripotiwa katika jariba la Bild.” Alisema Wenger

“Hakukua na mazungumzo yoyote kati yangu na mwenyekiti wa Bayern Munich, na nimeshangazwa kwa taarifa hizi, sijui zimetokea wapi.”

Bayern Munich kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya Bundesliga, ikiwa nyuma kwa alama nne dhidi ya Borussia Mönchengladbach wanaoongoza msimamo huo.

Bangura asamehe yaliyotokea Sierra Leone mwezi Septemba
Don Garber: AC Milan inamuwinda Zlatan Ibrahimovic