Timu ya taifa ya Argentina itacheza mchezo wake wa mwisho nyumbani wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia kwenye uwanja wa Bombonera unaomilikiwa na klabu ya Boca Juniors, tofauti na ilivyozoeleka kuwa timu hiyo hutumia uwanja wa Monumental uliopo Buenos Aires.

Uwanja wa Monumental unamilikiwa na mahasimu wa Boca Juniors, River Plate, kwa sasa umeonenakana hauna bahati na timu hiyo ambayo imezoeleka kushiriki fainali za kombe la dunia.

Sababu kubwa ya kubadilisha uwanja utakaotumika kwa ajili mchezo dhidi ya Peru mwezi ujao, ni kusaka bahati kwa timu hiyo kufanya vyema ili kufikia lengo la kufuzu fainali za 2018 zitakazounguruma nchini Urusi.

Hata hivyo kocha wa Argentina Jorge Sampaoli amehitaji timu yake kucheza katika uwanja mdogo wa Bombonera, kwa ajili ya kutaka kuona mashabiki wakiwa karibu karibu na kuishangilia timu yao kwa nguvu zote.

Argentina kwa sasa inakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi la ukanda wa kusini mwa Amerika na imesaliwa na michezo miwili dhidi ya Peru na Ecuador.

Mchezo dhidi ya Peru umepangwa kucheza Oktoba 05, ambapo shirikisho la soka nchini Argentina na mashabiki wa nchi hiyo wanaamini utakua ni wa kipekee, kutokana na kuhitaji kushinda ili kufufua matumaini ya kufuzu moja kwa moja, bila kupitia mchezo wa mtoano kwa kucheza dhidi ya mshindi wa Oceania (New Zealand).

Kikosi cha Argentina kilifika hatua ya fainali mwaka 2014 nchini Brazil, lakini hakikubahatika kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, kufuatia kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Ujerumani.

Manji afutiwa kesi ya uhujumu uchumi
Wabunge wa Jubilee wataka jaji mkuu ang'oke