Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amekanusha uvumi wa kumdhalilisha aliyekua mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo Jose Mourinho ambaye kwa sasa ni bosi wa kikosi cha Man Utd.

Conte alikanusha uvumi huo dakika chache baada ya mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England kati ya Chelsea na Man Utd kumalizika kwenye uwanja wa Stamford Bridge, ambapo wenyeji walichomoza na ushindi wa mabao manne kwa sifuri.

Meneja huyo kutoka nchini Italia alisema matokeo ya mchezo huo daima yatabaki kama yalivyo, na ameomba yasichukuliwe kama sehemu ya kudhalilishwa kwa Mourinho ambaye aliondoka klabuni hapo mwishoni mwa mwaka 2015.

Conte alilazimika kukanusha suala hilo, kufuatia mpinzani wake Jose Mourinho kusema bila uoga aliopozungumza na vyombo vya habari ambapo alibainisha kuwa Chelsea walipanga kumdhalilisha.

Mourinho alitumia kigezo cha kitendo cha Antonio Conte cha kuwahamasisha mashabiki wa Man Utd kushangilia ilihali alitambua hawawezi kufanya hivyo kutokana na hali ilivyokua ikiendelea uwanjani.

Mourinho anaamini Conte alifanya kitendo hicho kwa dhihaka dhidi yake pamoja na jopo zima la ufundi la Man Utd.

Mabao ya Chelsea katika mchezo huo yalifungwa na Pedro Rodriguez, Gary Cahill, Eden Hazard pamoja na N’Golo Kante.

Mourinho: Nimeumizwa Na Matokeo, Ninaipenda Man Utd 100%
Real Madrid Yazipiga Kumbo Sevilla CF, FC Barcelona