Bondia Anthony Joshua anatarajiwa kuongeza mamilioni ya fedha baada ya pambano lake dhidi ya Andy Ruiz Jr litakalofanyika Desemba 7, mwaka huu nchini Saudi Arabia.

Pamoja na hivyo, Joshua, bingwa wa zamani wa mikanda ya uzito wa juu ya WBA, WBO na IBF bado yuko nyuma kwenye suala la utajiri kwa mabondia kwa kuwa ameachwa mbali na bondia mstaafu na nguli, Floyd Mayweather.

Joshua atapanda ulingoni katika pambano hilo la marudio baada ya kupoteza awali kwa mpinzani wake huyo.

Mayweather anaongoza orodha ya mabondia ambao wana utajiri mkubwa licha ya kuwa kwa sasa hapandi ulingoni, lakini bado ana utajiri wa kiwango cha juu akiwa ana utajiri wa pauni 435m (Sh trilioni 1.2).

Kwenye orodha iliyotolewa hivi karibuni na Jarida la Forbes, inaonyesha kuwa Mike Tyson ambaye aliwahi kutamba miaka ya nyuma naye yumo kwenye orodha hiyo japo mambo yake siyo mazuri sana kama ilivyokua awali.

Kuna wakati alikuwa na utajiri wa pauni 233m (Sh bilioni 686), lakini baadaye ukashuka na ikaelezwa kuwa mwaka 2003 alitangaza kufilisika kutokana na mambo yake mengi kwenda kombo, baadaye alirejea kwenye mstari. Orodha kamili hii hapa:

FLOYD MAYWEATHER, PAUNI 435M, (SH TRILIONI 1.2) Ni Bondia ambaye alimaliza maisha yake ya ndondi bila kupoteza anashika namba moja. Amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuonyesha utajiri wake ikiwemo magari ya kifahari, saa, fedha na karatasi za benki.

Mwenyewe amejipa jina la utani la “The Money”. Mayweather, mara ya mwisho alipopanda ulingoni ilielezwa kuwa alilipwa pauni 200m kwa kupigana na Conor McGregor, likiwa ni pambano lake la 50 akishinda yote.

GEORGE FOREMAN ,PAUNI 233M, (SH BILIONI 686) Ni mkongwe ambaye alijulikana kwa mbinu nyingi na ubishi awapo ulingoni. Alistaafu ndondi mwaka 1997 akiwa ameshinda mapambano 76 kati ya hayo 68 yakiwa kwa KO huku akipoteza matano.

Baadaye alipostaafu akaelekeza nguvu zake kwenye biashara ya chakula, uandishi wa vitabu na ujasiriamali.

OSCAR DE LA HOYA, PAUNI 155M, (SH BILIONI 456) yeye baada ya kustaafu kupigana akiwa ameshinda mikanda 10 ya ubingwa katika uzito sita tofauti, akaamua kuelekeza nguvu zake kwenye upromota na huko ndiko umaarufu wake ulikoongezeka.

Anaiendesha Kampuni ya Golden Boy Promotions, aliwahi kuulizwa siri ya mafanikio akasema: “Zungukwa na watu walio makini zaidi yako.”

MANNY PACQUIAO, PAUNI 148M, (SH BILIONI 435) Umri wake ni miaka 40 lakini bado anapigana, akiwa na makali alipewa jina la Pac-Man lakini malipo yake makubwa zaidi ni wakati alipopigana na Floyd Mayweather, Machi 2, 2015.

Alipoteza pambano hilo kwa pointi lakini mwisho akapata pauni 100m (Sh bilioni 294). Amekuwa akisaidia jamii mara nyingi na pia ni mwanasiasa.

LENNOX LEWIS, PAUNI 109M, (SH BILIONI 321) Anatambulika kuwa mmoja wa mabondia bora kuwahi kutokea Uingereza, Lewis alifunika ngumi za uzito wa juu miaka ya 1990.

Alikuwa bingwa mara tatu, baadaye akaingia kwenye filamu, shoo za TV na kwa sasa anafanya mambo yake binafsi.

SUGAR RAY LEONARD, PAUNI 93M, (SH BILIONI 274)

Kwa sasa ni mhamasishaji, alishinda mataji katika uzito kwenye ngazi tano katika miaka 20 aliyocheza ndondi.

Kwa sasa amekuwa akialikwa kuchambua mapambano mbalimbali na kuchangisha fedha katika matukio ya kijamii.

CANELO ALVAREZ, PAUNI 73M, (SH BILIONI 218) Ni mwanamichezo wa nne nyuma ya Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Neymar kwa sasa katika malipo makubwa.

Hiyo inatokana na mkataba aliosaini na Kampuni ya DAZN wenye thamani ya pauni 284m (Sh bilioni 836).

Pambano lake lijalo ni dhidi ya Sergey Kovalev raia wa Urusi litakalofanyika Novemba 2. Canelo anakumbukwa na wengi kwa kupoteza pambano dhidi ya Mayweather mwaka 2013 kwa pointi licha ya mashabiki wengi kumpa ushindi yeye.

VITALI KLITSCHKO, PAUNI 62M, (SH BILIONI 183) Licha ya jina lake kufunikwa na mdogo wake, lakini bado Vitali alikuwa na ubora wa juu katika uzito wa juu. Ameshastaafu lakini ana utajiri mkubwa kuliko mdogo wake, Wladimir ambaye aliendelea kupigana kwa miaka kadhaa.

Vitali sasa ni mwanasiasa na ni Meya wa Kiev na pia ni mbunge wa zamani wa Ukraine.

WLADIMIR KLITSCHKO, PAUNI 47M, (SH BILIONI 138) Ubora wake ulizimishwa na Joshua katika pambano lake la mwisho kabla ya kustaafu. Akiwa na kaka yake walikuwa tishio kwenye ndondi miaka ya 1990.

ANTHONY JOSHUA, PAUNI 43M, (SH BILIONI 127) Pambano lake la marudio dhidi ya Andy Ruiz Jr ni gumzo, anatarajiwa kupata pauni 50m (Sh bilioni 147) katika pambano hilo ikiwa atashi-nda, inaweza kuon-geza kitu kwenye utajiri wake.

Jinsi ya kutumia kabichi kama dawa
Ndalichako awapa onyo maofisa elimu mikoa