Mahmoud Jibril, aliyekuwa kiongozi wa jeshi la waasi nchini Libya lililomuondoa madarakani alieyekuwa Rais wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi mwaka 2011, amefariki kwa virusi vipya vya corona (covid-19).

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na chama chake, Jibril aliyekuwa na umri wa miaka 68 alifariki Jumapili, Aprili 5, 2020 akiwa anapatiwa matibabu baada ya kulazwa hospitalini kwa kipindi cha wiki mbili jijini Cairo.

Katibu wa Chama cha National Forces Alliance, Khaled al-Mrimi ameeleza kuwa Jibril alilazwa katika hospitali maalum ya Ganzouri tangu Machi 21, 2020 baada ya kubainika kuwa na virusi vya corona.

“Afya yake ilianza kuimarika juzi, lakini ilianza tena kuzorota na ilipofika saa nane mchana alipoteza maisha,” Aljazeera inamnukuu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Hisham Wagdy.

Jibril alikuwa mshauri wa masuala ya uchumi wa Serikali ya Gaddafi, lakini mwaka 2011 alijiunga na kundi la mapinduzi lililoiondoa madarakani serikali hiyo.

Aliongoza waasi walioungwa mkono na majeshi ya NATO ambayo kwa pamoja yalimuondoa na kumuua Gaddafi.

Alikuwa kiongozi wa serikali ya mpito hadi mwaka 2012 baada ya Libya kufanya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia baada ya miongo minne. Baada ya uchaguzi huo, chama chake kilikosa nafasi ya kuchagua Waziri Mkuu.

 

Niyonzima amkubali Balama Mapinduzi
Chui-milia akutwa na virusi vya corona