Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma jana alimpongeza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Sharmillah Sarwatt aliyekataa kusajili kesi iliyowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuhusu Spika wa Bunge, Job Nduga kumtaka Mdhibiti na Msajili Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Bunge.

Spika Ndugai alimtaka CAG kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhojiwa kuhusu kauli yake aliyoitoa alipozungumza na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa akidai kuwa, kama Bunge halizifanyii kazi ripoti zake, huo ni udhaifu wa Bunge.

Akizungumza jana na waandishi wa habari kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kushiriki Wiki ya Sheria itakayofanyika Januari 31 jijini Dodoma, Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakama ilitoa maelekezo kwa wasajili kutosajili kesi ambazo zina makosa ya kiufundi.

Alisema uamuzi huo unatokana na kuyafanyia kazi mapendekezo ya Wabunge pamoja na wananchi kuhusu kesi zinazotupwa baada ya kufika mbele ya Majaji kwa sababu tu zina makosa ya kiufundi badala ya kuangalia hoja husika.

“Ningependa kuchukua fursa hii kumpongeza msajili aliyesimama kidete na kukataa kesi yenye makosa, yenye dosari, ili ipelekwe kwa Jaji, ili Jaji aifute, airudishe tena. Huo ni ujasiri ambao tunataka wasajili wote wahakikishe kwamba kesi zenye dosari haziingii kabisa kwenye mfumo wa Mahakama,” alisema Jaji Mkuu.

Zitto Kabwe kupitia kwa Mwanasheria wake, Fatma Karume walitaka kusajili kesi ya kikatiba inayoiomba Mahakama kutoa ufafanuzi wa Ibara ya 143 (6) kuhusu madaraka ya CAG.

Naibu Msajili aliwaandikia barua akiwaeleza kuwa kesi yao haitasajiliwa kutokana na kuwa na makosa ya kiufundi ikiwa ni pamoja na kutoambatisha nakala ya wito uliotolewa na Spika kwa CAG.

Hata hivyo, baada ya kufanya marekebisho, walifanikiwa kuisajili kesi hiyo Jumatatu ya Januari 21, siku ambayo CAG aliitikia wito na kuhojiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

Siku iliyofuata, Kamati hiyo ilimhoji pia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuhusu kauli yake dhidi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Prof. Lipumba atangaza maombi
Anusurika kifo kisa marejesho ya mkopo