Mwanamke mmoja raia wa Australia amehukumiwa kifungo jela baada ya kukutwa na hatia ya kugushi wasifu wake wa taaluma na uzoefu (CV) uliomsaidia kupata kazi yenye malipo ya $185,000 (sawa na Sh. 425,028,435) kwa mwaka.

Veronica Hilda Theriault (46), pamoja na makosa mengine alibainika kuwa aligushi wadhamini (referees) na hatimaye alifanikiwa kupata kazi kama Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kimkoa nchini humo.

Kwa mujibu wa CNN, Bi. Theriault alikiri mahakamani kufanya kosa hilo mwaka 2017. Jana, Novemba 4, 2019 alihukumiwa kifungo cha miezi 25 jela kwa makosa ya udanganyifu na matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Katika nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, ilielezwa kuwa mwanamke huyo alibainika kuwa alitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu elimu yake na historia ya kazi alizowahi kufanya.

Jaji Michael Boyla alisema upelelezi ulibaini kuwa alidanganya pia mtandaoni kwa kuweka picha ya mwanamitindo nyota, Kate Upton kwenye ukurasa unaomtambulisha wa LinkedIn.

Aidha, baada ya kupata kazi alimuajiri kaka yake ambaye pia hakuwa na vigezo vya kazi husika. Hata hivyo, mwanamke huyo alibainika kuwa na matatizo kidogo ya kiakili.

Jaji Boyla, ingawa alifahamu tatizo la kiakili la mwanamke huyo, alisisitiza kuwa atakaa jela kwa kipindi alichopangiwa na kwamba makosa aliyoyafanya yameonekana kuwa yalipangwa vizuri.

Dovutwa apinga kuvuliwa uenyekiti UPDP
Watu milioni 3 waathirika na mvua Afrika Mashariki