Ali Kiba amekuwa msanii wa kwanza mkubwa Tanzania kuzungumzia hatua ya wasanii nchini kutotajwa katika orodha ya wanaowania Tuzo za BET mwaka huu, zitakazotolewa Juni 23, 2019, Los Angeles, Marekani.

Akifunguka kupitia The Playlist ya Times Fm, Ali Kiba ambaye miaka ya nyuma amekuwa mmoja kati ya wasanii waliotajwa kwenye tuzo kubwa za kimataifa, amesema kuwa kukosekana kwa jina la msanii wa Tanzania katika tuzo hizo kutawahuzunisha ambao wanafanya kazi wakijikita katika kutajwa kwenye tuzo hizo.

“Sio kwamba hatufanyi kazi bali inatakiwa tuongeze. Lakini vilevile inatokana na watu ambao wanafo-cus(wanajikita) kuwa katika BET na sio katika kazi. Kama unataka kufocus katika BET fanya kama wanavyotaka lakini kama unataka kufanya kazi ili kila mtu akukubali uwe relevant kila siku fanya muziki utakaomgusa kila mtu sio Mtanzania tu peke yake,” alisema Ali Kiba.

Bosi huyo wa RockStar Africa, amesema kuwa hakuna kosa lolote kwa wasanii wa Tanzania kutotajwa kwenye tuzo hizo.

Tuzo za BET mwaka huu zitakuwa sehemu ya kumpa heshima rapa Nepsey Hustle aliyeuawa kwa risasi, atapewa tuzo ya heshima ya ubinadamu kutokana na kazi aliyoifanya ya kusaidia jamii. Tuzo nyingine ambayo imeshatangazwa ni ya Mary J Blige ambaye atakabidhiwa tuzo ya Mafanikio katika Maisha ya Muziki (Lifetime Achievement Award). Mwimbaji huyo ameshauza zaidi ya nakala milioni 50 za muziki wake.

Katika hatua nyingine, mkali huyo wa ‘Seduce Me’ ameeleza kuwa anawakubali sana Aslay na Nuh Mziwanda kwa vipaji vyao na kwamba anaamini kama msanii wa muda mrefu, wasanii hawa ni sehemu ya watakaokuja kuchukua nafasi ya kupeleka mbele zaidi Bongo Fleva.

Hata hivyo, alisema kuwa ili waweze kutimiza lengo hilo, ni lazima waendelee kujitambua na kujikita katika kuhakikisha wanafanya muziki ambao unawagusa watu wanaowalenga, unaodumu na wenye maana.

Sudan kusini: Panga la kubana matumizi latua baadhi ya balozi kufungwa
Pacquiao ahofiwa kupata majeraha ya ubongo