Kiungo mshambuliaji kutoka nchini England na klabu ya Liverpool Alex Oxlade-Chamberlain, huenda akazikosa fainali za kombe la dunia, kufuatia jeraha alilolipata wakati wa mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya AS Roma.

Chamberlain amekua na msimu mzuri tangu alipotua Liverpool mwanzoni mwa msimu huu akitokea kaskazini mwa jijini London yalipo makao makuu ya Arsenal, na tayari alikua ameshaanza kupewa nafasi kubwa na mashabiki wa soka nchini England ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo, ambacho kitashiriki fainali za kombe la dunia zitakazoanza Juni 14 nchini Urusi.

Katika mchezo wa usiku wa kuamkia leo dhidi ya AS Roma, Chamberlain alipatwa na maumivu makali ya goti baada ya kugongwa na Aleksandar Kolarov dakika ya 15, hali iliyopelekea nyota huyo kutibiwa uwanjani kwa muda kabla ya kutolewa kwa machela.

Meneja wa majogoo wa jiji (Liverpool), Jurgen Klopp amethibitisha kuwa vipimo vya awali vinaonyesha kiungo ameumia kwa kiasi kikubwa, na anaamini taarifa hizo hazitopokelewa vyema na mashabiki wa timu ya taifa ya England.

“Oxlade-Chamberlain ameumia vibaya, na tumebakiwa na mechi chache muhimu ambazo tunahitaji kuwa na kikosi kamili.

“Bado tunahitaji sapoti kutoka kwa mashabiki, jana walijitokeza kwa wingi pia tunahitaji Jumamosi wajitokeze kwa wingi kama leo,” alisema Klopp.

Katika mchezo huo Liverpool walichomoza na ushindi wa mabao matano kwa mawili, yaliyofungwa na Mohamed Salah na Roberto Firmino walifunga mabao mawili kila mmoja na Sadio Mane akifunga moja.

Video: LHRC yazindua ripoti ya Wasiojulikana
Serengeti Boys watinga fainali Burundi