Kundi la kigaidi la A-l Shabaab lenye makazi yake nchini Somalia limesema kuwa limetekeleza mashambulizi makali katika moja kati ya kambi za jeshi la Serikali ya nchi hiyo katika eneo la Puntland.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imedai kuwa walitekeleza shambulizi hilo mapema alfajiri na kwamba waliwaua wapiganaji 61 wa vikosi vya jeshi la serikali na kuteka magari 16.

Hata hivyo, kwa mujibu wa BBC, waziri wa eneo hilo amekanusha idadi ya vifo iliyotolewa na kundi hilo, ingawa hakueleza chochote kuhusu idadi ya waliojeruhiwa.

Al-shabaab ambayo ni mshirika wa Al-Qaeda imekuwa ikitekeleza mashambulizi kadhaa ikilenga vikosi vya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya jeshi la muungano la Umoja wa Afrika. Januari mwaka huu, Al-Shabaab walivamia kambi ya jeshi la Kenya katika mji wa Kolbiyow na kudai kuwa waliwaua wanajeshi 50.

Kenya ni sehemu ya vikosi vya Umoja wa Afrika, vyenye wanajeshi takribani 18,000 nchini humo vinavyoisaidia serikali ya Somalia kupambana na kundi hilo la kigaidi.

Putin asema hakuna atakayenusurika vita ya Marekani na Urusi
Zitto, Profesa Kitila watofautiana kwa mara ya kwanza hadharani