Mwenyekiti wa kamati ya kampeni na uchaguzi Taifa, Joran Bashange amesema mchakato wa uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, hauwezi kuendelea kwa haki hasa baada ya wananchi kuonyesha hisia zao za kuichoka CCM katika hatua za awali katika uandikishaji wapiga kura.

Kufuatia hatua hiyo, Chama cha ACT – Wazalendo kimetoa masharti yake ili kiweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa mara baada ya kujiondoa kwa kutokuridhishwa na utendaji wa mchakato huo.

Masharti hayo ni;

  1. Mchakato wote wa Uchaguzi uanze upya: Lazima yote yaliyofanyika chini ya utaratibu wa sasa yafutwe, uchaguzi uahirishwe na mchakato wa uchaguzi uanze upya.
  2. Wasimamizi wa Uchaguzi wote walioharibu mchakato wa uchaguzi huu wawajibishwe ili kukomesha tabia hii inayoharisha amani ya nchi.
  3. Zitungwe Kanuni Mpya za Uchaguzi kwa maridhiano na makubaliano na Wadau wote hususani vyama vya siasa.
  4.  Iundwe Kamati Huru ya kusimamia Uchaguzi: Lazima maamuzi katika hatua zote za Uchaguzi yawe ya maridhiano na makubaliano ya vyama sio TAMISEMI, ambao hawana uhuru, uwazi na wala uwezo wa kutenda haki.
  5. Waziri Selemani Jafo aitishe kikao cha pamoja cha vyama vyote vya siasa ili kukubaliana juu ya namna ya kusonga mbele Kwa utekelezaji wa mapendekezo yetu hayo. Kinyume na hivyo sisi ACT Wazalendo hatutashiriki Uchaguzi huu wa Tarehe 24 Novemba, 2019.
  6. Kutokana na O-TAMISEMI kuwa Wizara iliyopo chini ya OFISI YA RAIS, tunamtaka Rais Magufuli afikirie upya kuiondoa ofisi hii Ikulu na kuirejesha kwa Waziri Mkuu kama ilivyokuwa awali ili ‘TAASISI YA URAIS IEPUKANE NA KASHFA ZA UHARIBIFU WA DEMOKRASIA NCHINI’.
  7. Tunatoa wito kwa Vyama vyote vya Siasa kutokubali hadaa ya Waziri Jafo na kutumia nafasi hii kuwa pamoja kudai Tume Huru ya Uchaguzi ili Uchaguzi wa mwaka 2020 usiwe na dosari tulizoshuhudia sasa. Bila Tume Huru ya Uchaguzi pasiwe na Uchaguzi wowote nchini. Viongozi wa Kitaifa wa vyama watoke na tamko la pamoja kutaka TUME HURU YA UCHAGUZI.

Pia amesisitiza kuwa bado msimamo wao ni kujitoa kwenye uchaguzi na kuwataka wanachama wote nchi nzima kuendelea kutekeleza agizo la Chama la kuandika barua za kujitoa kwenye uchaguzi.

Aidha ametoa wito kwa wanachama wetu kubaini wagombea bandia wa CCM waliopewa fomu kwa kugushi mihuri na barua za utambulisho maeneo kadhaa nchini ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.”

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Novemba 12, 2019
Wasomi kukosa ajira kwatajwa kuondoa utulivu wa kisiasa